1 John 4

Zijaribuni Hizo Roho

1 aWapendwa, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho mwone kama zimetoka kwa Mungu, kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea ulimwenguni. 2 bHivi ndivyo mnavyoweza kutambua Roho wa Mungu: Kila roho inayokubali kwamba Isa Al-Masihi amekuja katika mwili yatoka kwa Mungu. 3 cLakini kila roho ambayo haimkubali Isa haitoki kwa Mungu. Hii ndiyo roho ya anayempinga Al-Masihi, ambayo mmesikia kwamba inakuja, na sasa tayari iko ulimwenguni.

4 dWatoto wapendwa, ninyi mmetokana na Mungu, nanyi mmewashinda kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika ulimwengu. 5 eWao wanatokana na ulimwengu na kwa hiyo hunena yaliyo ya ulimwengu, hivyo ulimwengu huwasikiliza. 6 fSisi twatokana na Mungu na yeyote anayemjua Mungu hutusikiliza, lakini asiyetokana na Mungu hatusikilizi. Hivi ndivyo tunavyoweza kutambua Roho wa Kweli na roho ya upotovu.

Mungu Ni Pendo

7 gWapendwa, tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu. Kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. 8 hYeye asiyependa hamjui Mungu, kwa sababu Mungu ni pendo. 9 iHivi ndivyo Mungu alivyoonyesha pendo lake kwetu: Mungu alimtuma Mwanawe wa pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kupitia kwake. 10 jHili ndilo pendo: si kwamba tulimpenda Mungu, bali yeye alitupenda, akamtuma Mwanawe, ili yeye awe dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu. 11 kMarafiki wapendwa, kama Mungu alivyotupenda sisi, imetupasa na sisi kupendana. 12 lHakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote.Lakini tukipendana, Mungu anakaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu.

13 mTunajua kwamba twakaa ndani yake na yeye ndani yetu, kwa sababu ametupa sisi sehemu ya Roho wake. 14 nNasi tumeona na kushuhudia kwamba Baba amemtuma Mwanawe ili awe Mwokozi wa ulimwengu. 15 oKila akiriye kwamba Isa ni Mwana wa Mungu, basi Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. 16 pHivyo nasi twajua na kulitumainia pendo la Mungu alilo nalo kwa ajili yetu.

Mungu ni Upendo. Kila akaaye katika upendo hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake.
17 qKwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu. 18 rKatika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo.

19 sTwampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza. 20 tIkiwa mtu atasema, “Nampenda Mungu,” lakini anamchukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa maana kila mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, atampendaje Mungu asiyemuona? 21Naye ametupa amri hii: Yeyote anayempenda Mungu lazima pia ampende ndugu yake.
Copyright information for SwhKC